Ikiwa ni siku chache baada ya kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya Mtoto wa Africa, nimeandika insha hii ili tuendelee kutafakari pamoja dhana hii adhimu ya “Mtoto wa Afrika”.
Nauliza uko wapi Mtoto wa Afrika? Sio kwa sababu sikuoni, la hasha! ila ninashindwa kukutambua kati ya haya mabilioni ya watu. Kwa nini hauonekani? Ni wapi umejificha? Ni nani alikuficha ili usijitambue wewe ni nani? Nina maswali mengi kuliko majibu ndio sababu nauliza uko wapi ili unikate kiu yangu.
Huyu niliyeambiwa ni Mtoto wa Afrika, ninashindwa kumtambua. Huyu amesahau tabia njema alizofunzwa na wazazi/walezi wake. Amepuuza lugha yake, mila, desturi na tamaduni za watu wake badala yake amekumbatia na kuhusudu za majirani.
Huyu amemsahau Muumba wake na kuanza kuwaabudu watu na kuvitumikia vitu alivyovitengeneza mwanadamu. Ndio maana akiamka asubuhi hushika simu yake kabla/badala ya kumshukuru aliyemuumba kwa kumpa nafasi nyingine ya kuishi na kufanya mabadiliko. Amesahau kuwa uwajibikaji, utu wema na familia imara ndio nguzo ya ustawi wa jamii bora.
Huyu amepuuza kazi, bidii na staha badala yake amekumbatia anasa, starehe na lawama. Ana sababu chungu nzima za kumlaumu kila mtu kwa kushindwa kwake kasoro yeye mwenyewe. Huyu anatumia muda mwingi zaidi kujiburudisha kuliko anavyojipatia muda binafsi kuyatafakari maajabu ya ulimwengu, kutafuta maarifa, kuzienzi tunu za taifa lake na kuwasaidia wenye uhitaji.
Huyu amesahau jina lake, la watu wake na kujinasibu kwa majina ya kigeni yasio ya asili yake. Anapenda aitwe Angel hataki kuitwa Malaika. Anapendelea zaidi aitwe Diva sio Mrembo. Mara mwingine ‘King’, mwingine ‘The great’, wakati huku kwetu tunawaita wafalme na miamba kama yule wa kaskazini. Ila mimi ni nani kuwa hakimu?
Naomba usinielewe vibaya, sijasema unakosea ila ninachotaka nikusihi ni kuikumbuka asili yako. Nakusihi kuchunguza imani na mifumo uliyorithi. Chunguza kama bado inakufaa au inahitaji mtazamo mpya. Mchunguze uliyerithi kwake, chunguza kusudi lake halafu uchunguze matokeo yake. Mwisho, nikukumbushe hekima walizotuachia wahenga waliosema, "Jasiri haachi asili" na pia kwamba, "Mwacha asili ni mtumwa"
Nauliza tena, uko wapi Mtoto wa Afrika? Nina kiu na majibu kutoka kwako.